Taarifa kutoka Jijini Mwanza zinasema kuwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesitisha udahili na usajili wa wanafunzi wa shahada ya udaktari wa binadamu kwa mwaka wa masomo 2025/26 katika Chuo Kikuu cha Mwanza, kutokana na chuo hicho kukiuka masharti ya uwezo wa kudahili.
Akizungumza leo mkoani Mwanza, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika kuwa chuo hicho kilipokea wanafunzi wengi zaidi ya uwezo wake wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo idadi ya wahadhiri.
Kwa mujibu wa Profesa Kihampa, chuo hicho kilipaswa kudahili wanafunzi 60 pekee kama ilivyoidhinishwa na TCU, lakini kilichukua wanafunzi mara 10 zaidi ya idadi hiyo na kushindwa kufanya marekebisho licha ya kupewa maelekezo mapema.
“Hatua inayofuata ni chuo kuwapatia wanafunzi hao vibali vya kuhamia katika vyuo vingine vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi wa programu ya udaktari wa binadamu,” alisema.
Aliongeza kuwa wanafunzi ambao watataka kubadilisha mwelekeo wa masomo, watachaguliwa kujiunga na programu nyingine zinazopatikana katika vyuo watakavyohamishiwa.


