Abiria wanne, wakiwemo watoto wawili, wamepoteza maisha baada ya basi la kampuni ya Miza Express kupata ajali katika eneo la Kijiji cha Ngukumo, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Basi hilo lililokuwa likifanya safari zake kutoka Mpanda kuelekea Bariadi lilipata ajali majira ya saa 9:20 usiku, baada ya kuacha njia na kugonga vyuma vya kingo za barabara kabla ya kupinduka na kutumbukia bondeni kilomita chache kabla ya kufika makao makuu ya Wilaya ya Nzega.
Baadhi ya abiria walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega kwa ajili ya matibabu, huku wengine waliokuwa wamenasa ndani ya basi wakilazimika kuokolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Twawa Juma Lulengelule, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema waliofariki ni wanaume watatu na mwanamke mmoja. Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa dereva alikosa umakini na kushindwa kulimudu gari hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda Twawa, kushindwa kulimudu basi kulisababisha litoke nje ya barabara, kugonga vyuma vya kingo za barabara na hatimaye kupinduka na kutumbukia bondeni. Uchunguzi zaidi unaendelea kubaini mazingira kamili ya ajali hiyo pamoja na hali za majeruhi.

