Ujenzi wa daraja la kisasa linalounganisha Kata za Matongo na Kibasuka wilayani Tarime unatarajiwa kumaliza tatizo la muda mrefu la ajali na vifo vilivyokuwa vikitokea wakati wananchi na wafugaji wakivuka mto kwa kutumia kivuko kisicho salama.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, amesema daraja hilo litakuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto iliyokuwa ikikwamisha shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo hayo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara ya kukagua miradi ya maendeleo, Chandi alisema wananchi walikuwa wakilazimika kutumia kivuko cha kamba kuvuka mto, hali iliyokuwa hatari zaidi wakati wa mvua.
“Kwa miaka mingi wananchi walikuwa wakikumbana na changamoto kubwa wakati wa kuvuka mto huu. Wakati wa mvua, maji yalikuwa yakiongezeka kwa kasi na kusababisha ajali mbalimbali, zikiwemo za kupoteza maisha ya watu pamoja na mifugo,” alisema Chandi.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha usafiri wa watu na bidhaa, kuimarisha usalama wa wananchi na kuongeza fursa za biashara na uwekezaji katika maeneo ya 7Matongo, Kibasuka na vijiji vya jirani.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi huo, Mhandisi Derrick Sira, alisema daraja hilo lenye urefu wa mita 41.5 limefikia asilimia 98 ya utekelezaji.
Amesema mradi huo umegharimu Shilingi milioni 400.6 kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia na unatekelezwa na kampuni ya Nyanjatec Contractors Limited.
“Kilichobaki kwa sasa ni kazi za mwisho za ukamilishaji pamoja na ukaguzi wa mwisho kabla ya wananchi kuanza kulitumia rasmi daraja hili,” alisema Mhandisi Sira.
Wananchi wa eneo hilo wameeleza matumaini kuwa mradi huo utaondoa adha ya kuvuka mto katika mazingira hatarishi na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kijamii na kiuchumi baada ya miaka mingi ya changamoto za usafiri.

