Msafara wa Vodacom Twende Butiama 2024 uliokamilika rasmi mnamo tarehe 13 Oktoba kwa mafanikio makubwa, ulihitimishwa wilayani Butiama, kijijini kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere katika mkoa wa Mara. Msafara huo, uliowakutanisha waendesha baiskeli zaidi ya 100 kutoka Tanzania na nchi jirani, ulifanyika kuanzia tarehe 29 Septemba na kupita katika mikoa 12 ya Tanzania.
Mafanikio ya msafara huu ni pamoja na kutoa huduma za afya bure kwa maelfu ya wananchi katika kambi za matibabu zilizowekwa njiani. Zaidi ya madawati 1000 yalichangwa kwa shule mbalimbali zikiwemo shule zinazohudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum, huku miche 50,000 ya miti ikipandwa katika maeneo mbalimbali ambako msafara huu ulipita, lengo likiwa ni uhifadhi wa mazingira.

