Vijana Jennifer Jovin (26) maarufu ‘Niffer’ na Mika Chavala waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhaini wameachiliwa huru mchana huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam.
Hatua hiyo imefikiwa leo wakati shauri hilo lilipopelekwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya kwa ajili ya kutajwa ambapo Wakili wa Serikali, Titus Aron alidai shauri hilo lilipelekwa kwa ajili ya kutajwa lakini DPP Sylvester Mwakitalu kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 92(1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai CPA hana nia ya kuendelea kuwashitaki washtakiwa wote wawili.
Baada ya kuelezwa hayo Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala alidai wamesikia na hawana pingamizi katika hilo kwakuwa ndiyo sheria inavyoelekeza hivyo alidai anaiomba mahakama iweze kutamka kwamba washitakiwa wameachiwa.
Hakimu Lyamuya aliwaeleza Washtakiwa kuwa upande wa mashitaka umewasilisha ombi la kuwafutia mashitaka chini ya kifungu kilichotajwa hivyo Mahakama inakubali ombi hilo na kueleza kuwa imewaachia huru Washitakiwa isipokuwa kama watashikiliwa kwa kosa jingine.


