Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limesikitika kutangaza kifo cha baharia raia wa Tanzania, ndugu Mchama Maregesi Mongu kilichotokea Mei 03, 2026 wakati akihudumu katika meli ya kuvuta (tug boat) iitwayo VOLANS yenye Namba ya Usajili ya Shirika la Bahari Duniani – IMO 929856, iliyobeba Bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), chombo hicho kilikuwa safarini kutoka nchini UAE kuelekea nchini Oman. Chombo hicho kilishambuliwa na bomu wakati kikivuka kwenye Mfereji wa Hormuz uliopo kati ya nchi za Iran na Oman.
Kipekee, TASAC inatoa pole za dhati kufuatia msiba huu na inaungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya kupoteza mpendwa wao.
Kwa sasa, TASAC kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinafuatilia kwa karibu taarifa za tukio hili ili kuweza kuurudisha mwili wa marehemu nchini mara tu mwili huo ukipatikana.
TASAC inaungana na IMO kusisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya mabahariawanapokuwa baharini, hususan katika maeneo yanayohusisha haki ya kupita kwa amani (innocent passage) kama inavyolindwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (UNCLOS).

